TOFAUTI KATI YA WANAZUONI
(INTELLECTUALS) NA WASOMI (INTELLECTS)
Mwanazuoni ni nani? Je, kuna tofauti kati ya mwanazuoni
(intellectual) na msomi (intellect worker/intelligentsia)?
Ndiyo, ipo tofauti. Wanazuoni wote, au karibu wote, ni wasomi
lakini siyo wasomi wote wanakuwa wanazuoni. Mara moja moja inatokea kwamba mtu
ambaye hajawahi kusoma katika taasisi yeyote ya elimu huwa mpevu kifikra na kwa
hiyo huwa na sifa za mwanazuoni. Lakini hii ni nadra sana. Kwa kawaida
wanazuoni wengi huwa wasomi. Kwa hivyo, hatuna budi tuanze kwa kueleza wasomi
ni nani.
Msomi huishi kwa nguvu-akili wakati mvujajasho huishi kwa
nguvu-mwili. Kwa maneno mengine, mfanyakazi huishi kwa jasho lake lakini msomi
huishi kwa ubongo wake. Katika mfumo wa kibepari hii ni aina mojawapo ya
mgawanyo wa kazi. Na tofauti kati ya msomi na mfanyakazi ni kubwa na ya
kipekee. Inakuzwa, inatuzwa.
Msomi hujivunia utaalamu na uelewa wake. Na kusema ukweli wasomi
wanakubalika katika jamii kama wanataaluma ingawa utaalamu wao unaweza ukawa
mkubwa juu ya jambo dogo. Elimu ya kibwanyenye huigawanya taaluma katika
visehemu vidogo vidogo. Kwa hivyo, kwa mfano, msomi wa uchumi siyo mtaalamu wa
uchumi kwa ujumla, bali anaweza akawa mtaalamu wa fedha tu au wa sarafu tu na
asiwe na ufahamu wowote wa uchumi kwa ujumla.
Msomi wa sheria anaweza akawa mtaalamu wa masoko ya hisa tu.
Anawashauri wacheza “kamari” katika soko hili - ni wakati gani mwafaka wa
kununua hisa na wakati gani wa kuziuza ili kujiongezea faida na utajiri. Mfano
mmojawapo wa mtaalamu wa masoko ya hisa na fedha ni George Sorros, anajulikana
kama msomi aliyejitajirisha kwa kuhamishahamisha fedha kutoka soko moja kwenda
soko jingine. Baada ya kutengeneza faida na kutajirika kwa njia hii sasa
anafadhili mashirika yasiyo ya kiserikali ya kutetea mfumo wa demokrasia ya
kiliberali katika nchi nyingi, pamoja na Afrika.
Huyu ni msomi; anachuma fedha na kuishi maisha ya anasa na ya
heshima kwa kutumia akili zake “shupavu” za kucheza “kamari”. Wako wasomi wa
aina nyingi tu – wakuu wa mashirika ya biashara, wahandisi, wanasheria,
wanasiasa, wanaharakati, wahadhiri, watumishi wa ngazi ya juu katika serikali,
biashara, viwanda na wengine wengi. Lakini wengi hawa siyo wanazuoni. Wanazuoni
hutofautishwa na wasomi kwa sifa kama sita hivi.
Moja ni kwamba mwanazuoni huchambua mambo kihistoria. Tukio au
jambo limetoka wapi, liko wapi na linaelekea wapi. Mwongozo wake ni kuchambua
mielekeo. Tukifananisha na mpiga picha, tunaweza kusema kwamba mwanazuoni
hupiga video, sio picha. Hii haina maana kwamba kila mwanazuoni ni
mwanahistoria. La hasha! Haiwezekani. Lakini kila mwanazuoni ana mwelekeo wa
kihistoria katika uchambuzi wake.
Pili, na hili lina uhusiano wa karibu na hilo la kwanza, ni
kwamba anaangalia mambo – hususan ya kijamii – katika uhusiano wake na mambo
mengine. Kwa mwanazuoni, hakuna jambo lisiloingiliana na jingine. Kuweza
kuelewa mwingiliano ni muhimu, badala ya kulitenganisha tukio au jambo na
muktadha wake. Kwa mfano, huwezi kuelewa chanzo au vyanzo vya umaskini katika
jamii bila kuelewa historia yake na uhusiano wake na utajiri. Umaskini na
utajiri ni kama mapacha na vina historia moja. Matajiri wachache wananeemeka na
umaskini wa wengi. Kwa hivyo, kuna mwingiliano kati ya umaskini na utajiri.
Hata hivyo, baadhi ya wasomi huchambua umaskini bila kuangalia historia yake na
kuchukulia, bila kudadisi, kana kwamba umaskini umekuwepo tangu enzi za kale na
utaendelea kuwepo milele, isipokuwa labda unaweza kupunguzwa. Tuna mashirika
mengi yanayozungumzia upunguzwaji wa umaskini (poverty alleviation) badala ya
utokomezaji wa umaskini. Na huwezi kutokomeza umaskini bila kuelewa vizuri
chanzo cha umaskini, uhusiano wake na utajiri na mfumo wenyewe unaozaa matabaka
ya walionacho na wasionacho.
Tatu, mwanazuoni huamini kwamba ukweli haugawanyiki, the truth
is the whole. Maana yake ni kwamba huwezi kupata ukweli wa jambo kama
hujaliangalia jambo hilo katika muktadha wake. Nikitoa ule mfano maarufu,
huwezi ukasema kwamba tembo ni kama kamba nene kwa sababu umegusa mkia wake au
kwamba tembo ni mpana kwa sababu umegusa sikio lake. Ili kujua ukweli wa umbo
la tembo ni lazima uangalie umbo lake zima. Nitoe mfano mwingine. Ukitaka
kuchambua muundo wa kiti, huwezi ukachambua miguu yake tu. Wala huwezi kusema
kwamba sehemu za kiti ni miguu na sehemu za kukalia na kuegemea. Ukijumlisha
sehemu hizo hutapata kiti, utakachopata ni rundo la mbao! Ukitaka kuelewa
muundo wa kiti kizima, huna budi uchambue jinsi na katika uhusiano upi, sehemu
zake zote zimeunganishwa.
Nne, mwanazuoni ni wakala
wa mabadiliko ya hali iliyopo, na siyo mtumwa wake. Dhamira yake ni kuigeuza na
siyo kuigandisha hali iliyopo. Dhamira yake ni kuleta hali bora katika jamii,
hususan kwa walio wengi. Yeye daima ni mpambanaji. Anapambana dhidi ya dhuluma,
uonevu, ukandamizaji na uovu mwingine popote pale ulipo. Ndiyo dhamira yake,
ndiyo maisha yake, ndiyo uhai wake. Anajitambulisha na wapambanaji wenzake bila
kujali wanakotoka, makabila yao, au rangi yao. Jamaa mmoja alimwandikia Che
Guevara kwamba kutokana na majina yao kufanana labda wao ni ndugu wa damu. Che
alimjibu kwamba yeye haoni kwamba wao ni ndugu: ‘Lakini’, namnukuu, ‘kama wewe
unachukia uonevu popote pale ulipo, basi sisi ni ndugu, makamaradi …. bila
kujali kama sisi ni ndugu wa damu’.
Tano, mwanazuoni hujali na kupigania maendeleo ya wanadamu,
maendeleo ya wote, siyo ya wachache. Sita, ili kukidhi uelewa wa jamii na
mazingira yake na ya ulimwengu, mwanazuoni hujikita kwenye uchambuzi wa kina,
uchambuzi ambao unaongozwa na nadharia iliyopevuka. Ndiyo maana wanazuoni
wengi, hususan wa Afrika, wanavutiwa zaidi na nadharia ya kimapinduzi ya
usoshalisti. Kwa mwanazuoni huyo, ufahamu/elimu ni zana ya kukosoa hali ilivyo
bila kusita na kuielekeza kwenye kubadili jamii, siyo bidhaa ya kuuzwa. Katika
kusisitiza umuhimu wa nadharia ya kimapinduzi Amilcar Cabral, mkombozi na
kiongozi wa Guinea Bissau, alisema: ‘Bila nadharia ya kimapinduzi hakuna
mapinduzi yatakayoshinda’. Ni wazi kwamba sio kila mwanazuoni ana sifa hizo
zote kama itaeleweka vizuri zaidi katika sehemu inayofuata kuhusu wanazuoni na
matabaka ya kijamii. Wanazuoni wa tabaka Wanazuoni ni sehemu ya jamii na wana
uhusiano na jamii. Hawawezi kudai kwamba wao ni wachambuzi tu wa mambo na
kwamba taaluma yao haiguswi kwa namna yoyote ile na matakwa, hofu, hisia,
matumaini, fikra, itikadi na mitazamo ya jamii. Kwa kuwa jamii yenyewe ya
kibepari imegawanyika katika matabaka na makundi basi wanazuoni pia huwa
wasemaji wa tabaka fulani au kundi fulani, ama bila kujua au bila ya
kujitangaza.
Tabaka linalotawala hutawala pia mawazo, fikra na itikadi, ndiyo
maana katika mfumo wa kibepari itikadi ya kibwanyenye hutawala. Wanazuoni na
wasomi wengi hutumikia tabaka-tawala kwa njia moja au nyingine kwa kujenga na
kusambaza itikadi yao. Hata hivyo, wanazuoni wachache hutamani kujiunga na
wanyonge na kuwatetea. Hao ndiyo wanazuoni wa kimapinduzi. Hakuna mwanazuoni au
msomi asiyejikita ama kwenye tabaka-nyonyaji au tabaka-nyonywaji. Wote hujikita
kwenye tabaka fulani hata kama hawajitambui au kujitambulisha hivyo. Na mara
nyingi, unaoonekana kama mgongano wa kimawazo au kinadharia ni mgongano wa
mtazamo uliojikita kwenye tabaka au kundi fulani.
Mwanazuoni hufanya uchambuzi wa kijamii ili ayaelewe vizuri
mazingira kwa shabaha mahsusi ya kuboresha hali ya maisha ya walio wengi. Yeye
huanika uovu wote hadharani bila kujipendekeza. Katika hili uchambuzi wake
unakuwa kamilifu bila kujali utamfurahisha nani na utamuudhi nani, na hata kama
akisakamwa na wenye mamlaka na madaraka katika jamii, - wakiwemo watawala wa
kisiasa au watawala watarajiwa au watawala wa kiuchumi, - hasiti kusema ukweli
kama uchambuzi wake unamuelekeza kufanya hivyo.
Kwa vyovyote vile,
mwanazuoni mwanamapinduzi hawezi kukosa kuchukiwa na watawala na wenzao wa
tabaka la kisiasa, political class. Kama mwanafalsafa wa kimapinduzi Karl Marx
alivyosema: “It is certainly not our task to build up the future in advance and
to settle all problems for all time, but it is just as certainly our task to
criticise the existing world as ruthlessly in the sense that we must not be
afraid of our own conclusions and equally unafraid of coming into conflict with
the prevailing powers.” Kwa muhtasari, anachosema Marx ni kwamba kwa hakika
siyo kazi ya wachambuzi au wanafalsafa kutanguliza kujenga mustakabali na
kutatua matatizo yote kwa enzi zote, lakini ni kwa hakika pia kazi yao ni
kukosoa hali ya ulimwengu iliyopo wakati huo bila kusita na kutokuhofia matokeo
ya uchambuzi wao hata kama haya yatawaingiza kwenye misuguano na wenye
madaraka.
Niongeze kusema kwamba ni wazi kabisa kwamba wanazuoni
wanaotetea hali ilivyo bila shaka hawatakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa
wale wanaofaidika na hali hiyo. Kwa upande mwingine, wale wanaotaka kubadili
hali kwa mtazamo wa wavujajasho watakuwa na hali ngumu, watasakamwa,
watatungiwa uongo, watadhalilishwa na hata kujeruhiwa au kuuawa. Kwao hii siyo
hoja. Katika misitu ya Bolivia, wakati Che Guevara alipokutana ana kwa ana na
wanajeshi mamluki wa Serikali, mmoja wao alimtambua na kulenga bastola yake
kwake. Lakini alikuwa anasitasita kuifyatua. Che akamwambia, kwa sauti ya
utulivu; ‘Unasita nini. Fyatua risasi yako, utakuwa umemuua mtu tu!’, kwa maana
kwamba huwezi kuua fikra na mtazamo wa mwanamapinduzi na kweli kabisa mpaka leo
fikra za Che zimedumu.
Katika historia yetu ya mapambano ya ukombozi tuna mifano mingi
ya wanazuoni waliojitolea mhanga kwa sababu ya msimamo wao kuwa upande wa umma.
Patrice Lumumba alitaka nchi yake iwe na uhuru kamili ili iweze kutumia utajiri
wake kwa manufaa ya, siyo Wakongomani tu, bali kwa manufaa ya watu wa Afrika
kwa sababu Lumumba alikuwa muumini wa Umajumui wa Afrika (Pan-Africanism).
Aliuawa kikatili na wakala wa CIA.
Kwame Nkrumah wa Ghana aliuchambua na kuukusoa mfumo wa
ukandamizaji wa kibeberu, akitaka kuleta Umoja wa Afrika kwa sababu aliamini
kabisa kwamba wananchi wa vinchi vya Afrika wakiwa peke yao, hawataweza kumudu
nguvu za kibeberu. Akapinduliwa na waliochukua madaraka kama mwanajeshi Afrika
aliyekuwa na mawazo finyu, wakamsakama na kumdhalilisha. Chris Hani, ambaye
alikuwa na dhamira ya kujenga Afrika Kusini mpya kwa mtazamo wa wavujajasho,
aliuawa katika kipindi nyeti cha mpito kutoka ukaburu kwenda ukombozi. John
Garang, kiongozi wa muda mrefu wa Sudan Kusini, alikuwa na msimamo wa
kutokutenga na kuvunja nchi ya Sudan, badala yake alitaka Sudan Mpya. Umma wa
Sudan Kusini na Sudan Kaskazini walikuwa nyuma yake. Inasemekana alikufa katika
ajali ya helikopta. Sina hakika!
Muammar Gadaffi, mwanasiasa aliyekuwa na dhamira ya kuleta
mabadiliko makubwa na yenye maslahi kwa nchi na jamii yake, ingawa baadaye
alianza kuyumbayumba, aliuawa na majeshi ya mamluki yakisaidiwa na NATO. Kosa
lake? Alikuwa na mpango kabambe wa kuvuna maji yaliyopo chini ya ardhi ya
jangwa la Sahara na kueneza maji hayo katika eneo lote la Sahel. Lakini Rais wa
Ufaransa, wakati ule Sarkozy, alikuwa na mpango wake mbadala. Alitaka Gadaffi
akubali kutoa idhini ili mashirika ya Kifaransa wayavune maji hayo na
kuyasafirisha kwenda Ufaransa kwa ajili ya kutengeneza maji ya chupa. Gadaffi
alikataa katakata. Akasukiwa mpango, nchi yake ikavamiwa na hatimaye akauawa.
Leo hii nchi ya Libya imesambaratishwa na hao hao waliojiita wakombozi. Nchi na
vyombo vya habari vya Magharibi waliwakuza sana vibaraka hao na kuwatambua kama
“wakombozi”, ili kuhalalisha maslahi yao ambayo yalikuwa sababu kuu ya
kumpindua na kumuua Gadaffi.
BY ISSA SHIVI
GAZETI LA RAIMWEMA TOLEO NAMBA 351
MAY 7, 2014
Safi sana hii
ReplyDelete